KESHA LA ASUBUHI
NJONI KWANGU – Aprili 1
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Mathayo 11:28. Wengi wanaosikia mwito huu, wanatamani sana kupumzika, lakini wanazidi kusonga mbele katika njia ile inayoparuza, wakiwa wameikumbatia mizigo yao karibu sana na moyo wao. Yesu anawapenda, naye anatamani sana kuibeba mizigo yao pamoja na wao wenyewe katika mikono yake yenye nguvu. Angependa kuziondoa hofu zao na mashaka yao yanayowanyang'anya amani na pumziko; lakini hawana budi kwanza kuja kwake, na kumweleza shida zao za siri zilizomo mioyoni mwao. Wakati mwingine tunasimulia shida zetu zote masikioni mwa wanadamu, na kuwaeleza wale wasioweza kutusaidia katika mateso yetu, na kuacha kumweleza Yesu siri zetu zote, yeye awezaye kuigeuza njia ile inayotuletea majonzi na kutuingiza katika njia zake za furaha na amani.
Anatushauri sisi ya kuwa yeye ndiye rafiki yetu, awezaye kutembea pamoja nasi katika njia zetu zote za maisha zinazoparuza. Anatuambia, Mimi ni Bwana Mungu wako; tembea nami, nami nitaijaza njia yako na nuru. Yesu, Mfalme Mtukufu wa Mbinguni, anakusudia kuwainua katika hali ya kirafiki pamoja naye wale wote wanaokuja kwake pamoja na mizigo yao, udhaifu wao, na matatizo yao...Mwaliko wake kwetu ni mwito kwetu tupate kuishi maisha safi, matakatifu, na ya furaha. Maisha ya amani na raha, ya uhuru na upendo na kupata urithi tele mwishoni, yaani, ule uzima wa milele. Ni haki yetu kila siku kuwa na matembezi ya amani, ya karibu, na ya furaha pamoja na Yesu. – ST, Machi 17, 1887.
Pumziko [raha] linapatikana wakati kunapotupiliwa mbali kujihesabia haki kote, yaani, hoja zote zitokanazo na msimamo wa ubinafsi. Kujisalimisha nafsi kabisa, kuzikubali njia zake, hiyo ndiyo siri ya pumziko kamili katika pendo lake.... Fanya yale tu aliyokuambia kufanya, nawe uwe na hakika kwamba Mungu atafanya yote aliyosema atafanya. Je, umekuja kwake, na kuyaacha mambo yako yote uliyoyaweka badala yake, umeacha kutokuamini kwako kote, pamoja na kujihesabia haki wewe mwenyewe? Njoo kwake jinsi ulivyo, dhaifu, usiyejiweza, na uliye tayari kufa. Hivi "pumziko" lile lililoahidiwa ni pumziko gani? Ni kule kujua ya kwamba Mungu ni wa kweli, kwamba hamkatishi tamaa mtu ye yote anayekuja kwake. Msamaha wake ni tele na wa bure, na kule kukubaliwa naye humaanisha pumziko [raha] moyoni mwako, yaani, pumziko katika pendo lake. ----- RH, Aprili 25, 1899.
PUMZIKO KWA WALE WASIOTULIA
Aprili 2
Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali. Isaya 30:15. Yesu anakupenda wewe, naye anataka upendo wako. Angependa wewe ukumbuke kwamba alikutolea maisha yake ya thamani ili usipotee [usiangamie]; na ya kwamba kwako atakuwa msaada tele wakati wa shida. Wewe umwangalie tu Yesu na kumweleza kila tatizo ulilo nalo pamoja na maonjo yako. Mwombe akusaidie, kukutia nguvu na kukubariki, nawe amini kwamba anayasikia maombi yako. Mbingu yote inakuangalia wewe kwa hamu kubwa. Mtu mmoja ambaye Kristo amemfia ana thamani kuliko ulimwengu wote. Natamani kila kijana wa kiume na wa kike aweze kutambua thamani ya roho ya mwanadamu. Iwapo wangejitoa wenyewe kwa Yesu jinsi walivyo, ingawa ni wenye dhambi na wachafu, yeye atawakubali dakika ile ile wanapojitoa wenyewe kwake, na Yesu atatia Roho wake ndani ya moyo wa Yule mtafutaji mnyenyekevu.
Ye yote ajaye kwake hatamtupa nje kamwe. Unaweza kumpenda Yesu kwa moyo wako wote, naye hatakuangusha katika upendo wako huo na matumaini yako. Maneno yake ni uzima, faraja, na tumaini. Shetani anajua kwamba yote unayotakiwa kufanya ni kumtazama Yesu, Mwokozi wako aliyeinuliwa juu. Mtu Yule aliyejeruhiwa, aliyechubuliwa, na kupigwa atapata zeri [dawa ya kuponya] kwa majeraha yake ndani ya Yesu. Patakuwa na amani, yaani, amani ya kudumu, ikibubujika moyoni, maana pumziko hilo linapatikana kwa kujinyenyekeza kabisa kwa Yesu Kristo. Utii kwa mapenzi ya Mungu huleta pumziko hilo. Mwanafunzi yule anayekanyaga katika nyayo za Mkombozi wake mpole na mnyenyekevu anapata pumziko [raha] ambalo ulimwengu huu hauwezi kumpa, wala ulimwengu huu hauwezi kuliondoa. "Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini." Isaya 26:3. – Letter 6, 1893. Unyenyekevu na upole wa moyo, ambao daima ulikuwa ni tabia ya maisha matakatifu ya Mwana wa Mungu, ukiwa ndani ya wafuasi wake wa kweli, huleta hali ya kuridhika, amani, na furaha ambayo huwainua juu ya utumwa ule wa maisha ya unafiki. – HR, Desemba, 1871.
"MJIFUNZE KWANGU"
Aprili 3
Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Mathayo 11:29. "Mjifunze kwangu," alisema yule Mwalimu wa Mbinguni, "kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo...." Yatupasa kujifunza kujikana nafsi, yatupasa kujifunza ujasiri, saburi, ushupavu, na upendo unaosamehe.... Iwapo tunayo imani ndani ya Yesu kama msaidizi wetu, iwapo macho yetu ya imani yanaelekezwa kwake kila wakati, basi, tutakuwa kama Yesu katika tabia zetu. Atakaa ndani ya mioyo yetu, nasi tutakaa ndani yake Kristo. Tukiwa tumevikwa haki ya Kristo, maisha yetu yanafichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Atakuwa mshauri wetu. Tukimwomba kwa imani, atatufungua ufahamu wetu. Mafundisho aliyotupa Kristo yatawekwa katika matendo. – MS 21, 1889. Kristo, Kielelezo Chetu, anapowekwa daima mbele ya macho ya akili zetu, hapo ndipo tabia mpya zitaweza kukuzwa, mielekeo yetu mibaya yenye nguvu tuliyorithi pamoja na ile tuliyojizoeza wenyewe itaweza kudhibitiwa na kushindwa, kujisifu kwetu kutatupwa mavumbini, tabia mbaya za zamani za mawazo zitapingwa daima, kupenda kwetu makuu kutajionyesha katika tabia yetu kwa dhahiri na kudharauliwa, nasi tutakushinda. – MS 6, 1892.
Kristo hana budi kuingia katika mawazo yetu yote, hisia zetu zote, na mapenzi yetu yote. Anapaswa kutukuzwa katika mambo madogo sana ya utumishi wetu wa kila siku katika kazi ile aliyotupa kufanya. Wakati tunapoketi miguuni pake Yesu, badala ya kutegemea ufahamu wetu wa kibinadamu au kufuata maneno ya hekima ya ulimwengu huu, tunapaswa kuyapokea maneno yake kwa shauku, tukijifunza kwake, na kusema, "Bwana, wataka mimi nifanye nini?" hapo ndipo hali yetu ya asili ya kujitegemea wenyewe, yaani, kujitumainia wenyewe, kufuata mapenzi yetu wenyewe, itabadilika, na mahali pake itakuwapo roho ile ya kitoto, tiifu, inayokubali kufundishwa. Tunapokuwa na uhusiano sahihi na Mungu wetu, tutaitambua mamlaka ya Yesu katika kutuongoza sisi, na madai yake kwetu kwamba tumpe utii usiokuwa na maswali. – Letter 186, 1902. Tutakuwa na mawazo ya hali ya juu kumhusu Yesu Kristo hata nafsi zetu zitajishusha chini. Mapenzi yetu yatakuwa ndani ya Yesu, mawazo yetu yatavutwa kwa nguvu kuelekea mbinguni. Kristo atakuwa hana budi kuzidi, wakati MIMI NINAPUNGUA. Tutajizoeza kuwa na wema ule ulio ndani yake Kristo, ili sisi tupate kuakisi kwa wengine mfano wa tabia yake. – MS 21, 1889.
KUJITIA NIRA YA KRISTO
Aprili 4
Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. Mathayo 11:30. Kujitia nira ya Kristo, maana yake kufanya kazi kulingana na njia zake, kuwa mshirika mwenzi pamoja naye katika mateso yake na taabu zake kwa ajili ya wanadamu waliopotea. – 5BC 1092. Katika kuikubali nira yake Kristo ile ya kujizuia na utii, utaiona kwamba imekuwa msaada mkubwa sana kwako. Kujitia nira hii kunakuweka wewe karibu na ubavu wake Kristo, naye anachukua sehemu ile iliyo nzito kuliko zote ya mzigo huo. – 5BC 1090. Nira na msalaba ni nembo zinazowakilisha jambo lile lile moja – kusalimisha mapenzi [nia] yetu yote kwa Mungu. Kujitia nira kunamwunganisha mwanadamu katika urafiki pamoja na yule mpendwa sana Mwana wa Mungu. Kuuinua msalaba juu kunaiondoa nafsi moyoni, na kumweka mwanadamu mahali ambapo anajifunza kubeba mizigo yake Kristo. Hatuwezi kumfuata Kristo bila kujitia nira yake, yaani, bila kuuinua juu msalaba wetu, na kujitwika na kumfuata. Kama mapenzi yetu hayapatani na matakwa yale ya mbinguni, basi, inatupasa sisi kuyakataa matakwa yetu, kuachana na tamaa zetu tunazozipenda sana, na kukanyaga katika nyayo zake Kristo. Wanadamu hujitengenezea nira ambazo huonekana kuwa ni nyepesi na za kupendeza kuvaa kwa ajili ya shingo zao wenyewe, lakini matokeo yake ni kwamba zinachubua vibaya mno. Kristo analiona jambo hilo, na kusema, "Jitie nira yangu. Nira ile unayoweza kuitia shingoni mwako, ukidhani inakufaa sana, haitakufaa hata kidogo. Jitie nira yangu, nawe ujifunze kwangu mafundisho ambayo ni ya muhimu kwako kujifunza." – 5BC 1090,1091.
Kazi yako sio kukusanya mizigo yako mwenyewe. Mara nyingi sisi tunafikiri kwamba tuna wakati mgumu katika kuibeba mizigo yetu, na mara nyingi mno mambo yanakuwa hivyo, kwa sababu Mungu hajaweka mpango wo wote kwa ajili yetu kuibeba mizigo hiyo; lakini tunapojitia nira yake na kuibeba mizigo yake, hapo ndipo tunaweza kushuhudia kwamba nira ya Kristo ni laini na mizigo yake ni myepesi, kwa sababu yeye ameweka mpango wa kuibeba hiyo [mizigo yake]. – 5BC 1091. Hata hivyo, nira hiyo haitatupatia sisi maisha ya raha na uhuru na kujifurahisha nafsi zetu. Maisha yake Kristo yalikuwa ni maisha ya kujitoa mhanga na kujikana nafsi kwa kila hatua [aliyokwenda]; na kwa upendo unaodumu daima kama ule wa Kristo, mfuasi wake wa kweli atatembea katika nyayo za Bwana wake; naye atakapokuwa anasonga mbele katika maisha haya, atazidi kujazwa na roho ile ile na maisha yale yale ya Kriato. – 5BC 1092.
KUJIFUNZA KATIKA SHULE YA KRISTO
Aprili 5
Ni nani amchaye BWANA? Atamfundisha katika njia anayoichagua. Zaburi 25:12. Yesu amefungua shule kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwapa mazoezi wateule wake, nao wanapaswa kuendelea kujifunza daima kuyaweka katika matendo mafundisho yale anayowapa, ili wapate kumjua kabisa. Wale wanaofikiri kwamba wao ni wema kiasi cha kutosha, wala hawafanyi kazi kwa bidii katika kuikamilisha tabia yao ya Kikristo, wataweka sanamu mioyoni mwao, nao wataendelea kutenda dhambi katika maisha yao mpaka dhambi kwao itaonekana kuwa si dhambi tena. Yesu anajitoa nafsi yake kwa kila mtu aliye mgonjwa, kwa kila mtu anayejitahidi kushinda. Roho Mtakatifu anamwombea kila mpiga mweleka mwaminifu, naye Kristo atayafanya maneno yake kuwa roho na uzima, yaani, kuwa uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila mtu aaminiye. Lakini wewe utashindwa kabisa utakapomruhusu Yule mwovu kuutawala moyo wako, yaani, kuyaongoza mawazo yako. Mungu hatadhihakiwa; hataukubali moyo uliogawanyika. Yeye anataka tumpe huduma yetu yote kwa moyo wetu wote. Amelipa fedha ya fidia yetu kwa kujitoa nafsi yake mwenyewe kwa ajili ya kila mwana na binti ya Adamu.
Kristo anayo madai juu ya kila mtu; lakini wengi huchagua maisha ya dhambi. Wengine hawataki kuja kwa Yesu ili awape uzima. Wengine husema, "Naenda, Bwana," kwa mwaliko wake, lakini hawaendi; hawajisalimishi nafsi zao kabisa ili kukaa ndani ya Yesu peke yake, ambamo ni uzima na amani na furaha isiyoneneka, yenye utukufu.... Je! hamtaamka na kuwa na hekima na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya umilele? Itafuteni neema yake Kristo kwa moyo wenu wote, kwa uwezo wenu wote, na kwa nguvu zenu zote. Mungu amewapa ninyi haki ya kumshikilia Yeye kwa njia ya maombi ya imani. Maombi yaliyojaa imani ndicho kiini cha dini safi, ni nguvu ya siri aliyo nayo kila Mkristo. Tafuta muda wa kuomba, kuyachunguza Maandiko, kuiweka nafsi yako chini ya nidhamu ya Yesu Kristo. Uishi kwa kuwasiliana na Kristo aliye hai, na mara tu unapofanya hivyo, atakuchukua na kukushika kwa mkono wake ulio imara ambao
hautakuachilia kamwe. – Letter 38, 1893.
KUJIANDAA KWA SHULE ILE YA JUU ZAIDI
Aprili 6
Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa. Zaburi 25:5. Wale ambao ni wana wa Mungu hapa duniani wanaketi pamoja na Yesu katika Shule ya Maandalizi, wakijitayarisha kupokewa katika Shule ile ya Juu Zaidi. Siku kwa siku tunatakiwa kila mmoja kufanya maandalizi yake mwenyewe; maana katika majumba yale ya kifalme kule juu hakuna ye yote atakayewakilishwa na mtu mwingine. Kila mmoja wetu anapaswa kuusikia yeye mwenyewe mwito ule usemao, "Njoni kwangu,... nami nitawapumzisha...." Bwana Yesu amekulipia ada ya mafundisho. Yote yakupasayo kufanya ni kujifunza kwake. Upole kama ule wa Kristo utakaoonyeshwa kwa matendo katika Shule ile ya Juu unatakiwa kuwekwa katika matendo na waumini wote, wazee kwa vijana, katika Shule hii ya Chini. Wale wote wanaojifunza katika shule hii ya Kristo wako chini ya mafunzo wakiongozwa na wajumbe wale wa mbinguni [malaika]; wala haiwapasi kamwe kusahau ya kwamba wao ni tamasha kwa ulimwengu huu, kwa malaika, na kwa wanadamu. Wanapaswa kumwakilisha Kristo. Wanatakiwa kusaidiana wenyewe ili waweze kufaa kuingia katika Shule ile ya Juu zaidi. Wanapaswa kusaidiana kila mmoja na mwenzake ili wapate kuwa watakatifu na wenye utukufu, na kulizingatia sana wazo lile la kweli linaloonyesha maana ya kuwa mtoto wa Mungu. Wanapaswa kusema maneno ya kutia moyo. Wanapaswa kuiinua juu mikono iliyo dhaifu na kuyafanya imara magoti yaliyolegea. Juu ya kila moyo panatakiwa kuandikwa maneno haya, kana kwamba ni kwa kalamu yenye ncha ya almasi, "Hakuna kitu cho chote ninachokiogopa, isipokuwa tu kwamba mimi sitaujua wajibu wangu, au nitashindwa kuutekeleza."... Moyo uliodhibitiwa, maneno ya upendo na upole, humletea heshima Mwokozi wetu. Wale wasemao maneno ya upole, maneno ya upendo, maneno yaletayo amani, watatunukiwa vizuri sana.... Tunapaswa kumruhusu Roho wake kuangaza katika maisha yetu ya nje ule upole na unyenyekevu wa moyo tuliojifunza kwake. – Letter 257, 1903. Yesu ndiye Mwalimu wetu Mkuu.... Anapenda sana, tena yu tayari sana kukuchukua wewe katika ushirika wa karibu sana na Yeye mwenyewe. Yu tayari kukufundisha jinsi ya kuomba kwa imani yenye matumaini na uhakika kama ile ya mtoto mdogo. Jiandikishe upya jina lako kama mwanafunzi wa shule yake. Jifunze kuomba kwa imani. Pokea maarifa yake Yesu. Je! wewe huwezi kuketi miguuni pake Yesu na kujifunza kwake? – Letter 38, 1893.
NGUVU HALISI YA NIA
Aprili 7
Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo. 2 Wakorintho 8:12. Dini iliyo safi inahusika na matumizi ya nia. Nia ni uwezo unaotawala katika maumbile ya mwanadamu, ikiuleta uwezo mwingine wote uliomo mwilini chini ya mamlaka yake. Nia si kuonja wala mwelekeo, bali ni uwezo wa kuamua la kufanya ambao unafanya kazi yake ndani ya wana wa wanadamu ama ukiwaelekeza kwenye utii kwa Mungu, ama kwenye uasi. [Bila shaka] wewe unatamani kuyafanya maisha yako kuwa kama vile ambavyo yangefaa kukuwezesha kuingia mbinguni hatimaye. Mara nyingi unakata tama unapojiona mwenyewe kuwa u dhaifu katika uwezo wako wa kimaadili [tabia], unajikuta u mtumwa wa mashaka, tena umetawaliwa na tabia na desturi za maisha yako ya zamani ya dhambi.... Ahadi zako [maazimio yako] ni kama kamba zilizotengenezwa kwa mchanga.
Daima utakuwa hatarini mpaka hapo utakapoielewa nguvu halisi ya nia yako. Unaweza kuamini na kuahidi mambo yote, lakini ahadi zako au imani yako haina maana yo yote mpaka hapo utakapoiweka nia yako nyuma ya imani yako na nyuma ya matendo yako. Kama wewe unapiga vita ile ya imani kwa uwezo wako wote wa nia yako, utashinda. Hisia zako, mvuto wako, mapenzi yako ya moyoni, mambo yote hayo hayaaminiki, kwa sababu hayawezi kutegemewa. Lakini wewe huna haja ya kukata tamaa.... Ni juu yako mwenyewe kuisalimisha nia yako kwa nia ile ya Yesu Kristo; nawe unapofanya hivyo, Mungu atakushika mara moja na kufanya kazi yake ndani yako ili upate kutaka na kutenda yale yampendezayo Yeye. Mwili wako wote ndipo utakuwa chini ya utawala wa Roho wake Kristo, na hata mawazo yako yatatawaliwa naye. Huwezi kuzitawala hisia zako, wala mapenzi yako ya moyoni, kama unavyotaka mwenyewe; lakini unaweza kuitawala nia yako [maamuzi yako], nawe [kwa njia hiyo] unaweza kufanya mabadiliko kamili katika maisha yako. Kwa kuisalimisha nia [mapenzi] yako kwa Yesu, maisha yako yatafichwa pamoja na Kristo katika Mungu na kuunganishwa na mamlaka ile ipitayo falme zote na mamlaka zote. Utakuwa katika nguvu yake; na nuru mpya, yaani, nuru ile ya imani iliyo hai, itawezekana kwako kuwa nayo. Lakini nia yako ni lazima ishirikiane na nia yake Mungu. Je! wewe hutasema, "Nitampa Yesu nia yangu, nami nitafanya hivyo sasa hivi," na kuanzia dakika hii hutakuwa upande wake Bwana kabisa? – 5T 13, 514